Harambee stars yarejea nyumbani

Image caption Victor Wanyama

Nohodha wa timu ya taifa ya soka ya Kenya na mcheza kiungo wa klabu ya Southampton, Victor Wanyama, amewaongoza wachezaji wengine wa tImu hiyo kuikashifu wasimamizi wa soka nchini Kenya, kwa maandalizi duni ya mechi yao ya kirafiki iliyopangiwa kuchezwa hiuto jana dhidi ya Sudan.

Akiongea baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, kutoka Khartoum pamoja wa wenzake, Wanyama alisema ni kosa wa FKF kuwashurutisha wachezaji wa kulipwa kusafiri safari ndefu kwa mechi ya ambayo haikupangwa vyema.

Wanyama ambaye aliondoka kuelekea uingereza, muda mfupi baada ya kuwasili mjini Nairobi, amesema wachezaji hao walipoteza muda wao kufanya mazoezi ya pamoja kwa kuwa hakuna mechi waliocheza.

''Ni kosa kubwa kwa FKF na SFF kuwaalika wachezaji na huku wakiwa hawajafanya matayarisho yoyote. Tumepoteza nafasi ya kufanya mazoezi ya vilabu vyetu ambavyo vina mechi ngumu wikendi hii'' Alifoka mchezaji huyo wa Southampton.

Kenya kufanya uchunguzi

Image caption Timu ya soka ya Harambee Stars

Miongoni mwa wachezaji wa kimataifa waliokuwa wamesafiri ili kujiunga na Harambee Stars ni pamoja na mshambulizi wa klabu ya AJ Ajaccio Dennis Oliech mwenzake wa Inter Milan, Macdonald Mariga, Johanna Omolo, Francis Kahata wa klabu ya KF Tirana, mcheza kuingo wa Mc Algiers, Edwin Lavatsa na mlinda lango wa Al taawuon David 'Cheche' Ochieng.

Naibu kocha mkuu wa Harambee Stars, James Nandwa amesema, kikosi chake kimehuzunishwa sana na tukio hilo na kusema kuwa huenda wachezaji wa kulipwa wasiwe na motisha ya kurejea nyumbani, kuichezea timu hiyo ikiwa tatizo hilo halitatatuliwa.

Hata hivyo msemaji wa shirikisho la mchezo huo nchini Kenya, amesema kuwa wao wanasubiri ripoti kutoka kwa kiongozi wa ujumbe huo kabla ya kutoa taarifa yoyote.

Aidha amesema watawasilisha malalamiko yao kwa Sudan kuhusiana na tukio hilo la kubadili uwanja utakaotumiwa bila kuwapasha habari.