Matumaini ya Arsenal yatumbukia nyongo

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Arsenal ikuchuana na Bayern

Arsenal imebanduliwa nje ya michuano ya kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya, licha ya kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja na mabingwa wa Bundes Liga, Bayern Munich.

Kufuatia sare hiyo Bayern sasa imejihakikishia nafasi katika robo fainali ya kombe hilo.

Bayern imefuzu kwa robo fainali hizo kwa jumla ya magoli matatu kwa moja, baada ya kushinda mechi ya awamu ya kwanza kwa magoli mawili kwa yai.

Hata hivyo mabingwa hao wa Ujermani wangeliwaadhibu zaidi vijana wa Arsene Wenger, lakini bao la Javi Martinez lilikataliwa na refa wa mechi hiyo, kwa misingi kuwa mchezaji huyo alikuwa amejenga kibanda katika eneo la wenyewe.

Bayern ndiyo ilioona lango la Arsenal, kabla ya Lukas Podolski kusawazisha.

Kipa wa Arsenal aliiepushia klabu yake aibu zaidi pale alipookoa mkwaju wa penalti uliopigwa na Thomas Muller.

Kuondolewa kwa Arsenal katika kinyang'anyiro hicho sasa kumewaacha na nafasi mbili pekee ya kumaliza ukame wao wa miaka tisa wa kutoshinda kombe lolote.

Arsenal ingali inawania kombe la FA na lile la ligi kuu ya Premier ingawa wako alama tisa nyuma ya vinara wa sasa Chelsea.