Esperance 5-0 Gor Mahia (8-2)

Image caption Wachezaji wa Gor Mahia wakijiandaa

Haythem Goeini aliifungia Esperance Spotive ya Tunisia mabao matatu na kuisaidia kuwanyamazisha mabingwa wa ligi kuu ya premia ya Kenya Gor Mahia mabao 5-0 katika mechi ya mkondo wa pili yakuwania ubingwa wa Afrika iliyochezwa katika uwanja wa Rades ulioko Tunis Jumatatu.

Kufwatia mvua hiyo ya mabao Esperance Spotive de Tunis imefuzu kwa hatua ijayo na ushindi mkubwa wa jumla ya mabao 8-2 .

Esperance Spotive de Tunis ilikuwa imeshinda mkondo wa kwanza iliyochezwa katika uwanja wa Nyayo Nairobi mabao 3-2.

Mechi hiyo ilichezwa jumatatu baada ya mvua kubwa iliyonyesha jumapili kulazimisha mechi hiyo kuahirishwa.

Kocha wa Gor Bobby Williamson hakujua kilichowapata vijana wake Goeini alipofungua mvua hiyo ya mabao katika dakika ya kwanza ya mechi hiyo .

Mshambulizi huyo aliongeza mengine mawili katika kipindi cha pili kabla ya Harrison Aful na Bouba Aminoo kukamilisha darasa hili la kandanda.

Esperance imeratibiwa kuchuana na Real Bamako ya Mali katika mkondo ujao .