Atletico Madrid yafuzu kwa robo fainali

Haki miliki ya picha
Image caption Diego Costa

Diego Costa amedumisha rekodi ya kufunga katika mechi zake zote wa kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya, msimu huu pale Atletico Madrid ilipoishinda AC Millan na kufuzu kwa robo fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1997.

Mshambulizi huyo, ambaye aliifungia Madrid bao la pekee katika mechi ya raundi ya kwanza, alivurumisha kombora kali baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Koke dakika ya pili.

Arda Turan naye alifunga la pili kabla ya Raul Garcia kuongeza la tatu.

Na ili kudhihirisha kuwa yuko katika hali nzuri kwa sasa, Diego Costa kwa mara nyingine tena aliliona nyafu za wapinzani wao na kufunga bao lake la pili katika mechi mechi.

Costa, ambaye aliichezea timu ya taifa ya Uhispania mechi yake ya kwanza, amefunga magoli saba katika mechi tano za kuwania kombe la klabu bingwa Ulaya msimu huu na amefunga magoli 29 katika mashindano yote aliyoshiriki.

Leo usiku kutakuwa na mechi mbili, Barcelona watakwaruzana na Manchester City nayo Bayer Leverkusen wakisafiri Ufaransa kuchuana na Paris Saint Germain.