Michuano ya UEFA hapatoshi leo

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Samuel Eto'o mchezaji wa Chelsea akishangilia moja ya magoli yake katika ligi kuu ya England

Kivumbi cha michuano ya Kombe la UEFA, kusaka klabu bingwa Ulaya, kinaendelea Jumanne wakati miamba wa England, Chelsea watakapopepetana na miamba wa Ufaransa Paris Saint Germain, PSG katika mchezo wa marudiano hatua ya robo fainali, ambapo Chelsea watakuwa wenyeji.

Chelsea inatarajia kumtumia mshambuliaji wao Samuel Eto'o mwenye umri wa miaka 33 ambaye katika mchezo wa awali ulipigwa mjini Paris, hakucheza kutokana na maumivu ya nyama za paja, lakini Jumatatu alifanya mazoezi.

Mshambuliaji wa pembeni Andre Schurrle, ambaye alitoka nje kutokana na maumivu katika mchezo dhidi ya Stoke Jumamosi huenda akawa imepona na kucheza mchezo wa leo Jumanne.

Chelsea, The Blues wanatarajia kubadilisha matokeo baada ya mchezo wa kwanza kupokea kipigo cha magoli 3-1.

Mchezaji kiungo John Mikel Obi alikosa mchezo dhidi ya Stoke kutokana na kuumia, lakini anaweza kucheza nafasi ya Ramires anayetumikia adhabu ya kadi au kuchukua nafasi ya Nemanja Matic.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Zlatan Ibrahimovic mchezaji wa PSG ya Ufaransa na timu ya taifa ya Sweden

PSG watacheza bila mshambuliaji wao hatari Zlatan Ibrahimovic, ambaye alitoka nje katika mchezo wa awali baada ya kuumia paja katika mechi ya awali katika uwanja wa Parc de Princes.

Raia huyo wa Sweden, ambaye ametikisa nyavu mara 40 katika ligi kuu ya Ufaransa, Ligue 1 msimu huunafasi yake itazibwa na Edinson Cavani.

Mshambuliaji huyo wa Uruguay, ambaye amejiunga na PSG kwa kitita cha pauni milioni £55, msimu wa kiangazi, ni mchezaji tegemeo katika timu ya PSG ya kocha Laurent Blanc anayetumia mfumo wa uchezaji wa 4-2-3-1.

"Cavani' si tu mshambuliaji anayebaki kupokea mipira katika eneo la hatari, bali pia huzuia, hutafuta mipira na huwatisha wapinzani, hilo ni jambo kubwa kwetu," anasema Blanc.

Michezo mingine ya UEFA Jumanne inazikutanisha timu za Borrusia Dortmund ya Ujerumani na Real Madrid ya Hispania. Katika mechi yao ya awali, Borrusia ilichezea kipigo cha magoli 3-0. Mchezo huo ulifanyika mjini Madrid.

Jumatano Manchester United itakuwa inakabiliana na mabingwa watetezi wa kombe la UEFA Bayern Munich ya Ujerumani katika mchezo wa marudiano katika uwanja wa Allianz Arena. Mchezo wa awali katika uwanja wa Old Trafford, timu hizo zilifungana goli 1-1.

Mchezo mwingine utakuwa kati ya Atletico Madrid na Barcelona. Timu hizo nazo zilitoka sare ya 1-1.