Liverpool, Chelsea hapatoshi England

Image caption Makocha Brendan Rodgers wa Liverpool na Jose Mourinho wa Chelsea

Ligi kuu ya England leo inaingia katika hatua muhimu wakati timu mbili za Liverpool na Chelsea zinazowania taji la ubingwa wa ligi hiyo zitakapovaana Jumapili.

Liverpool ambayo ilianza kwa kusuasua mwanzo mwa msimu huu wa ligi kuu ya England, mara imejikuta kuwa ndiyo timu inayohofiwa na kupewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 24 iliyopita.

Chelsea iliyo chini ya kocha wake mahiri Jose Mourinho, imejikuta ikitetereka katika michezo kabla ya kupambana na wapinzani wao Liverpool pale ilipokubali kufungwa na Sunderland mabao 2-1 na kuongeza pengo la pointi.

Liverpool inaoongoza ikiwa na pointi 80 baada ya kucheza mechi 35 sawa na mpinzani wake Chelsea yenye pointi 75. Nafasi ya tatu inashikiliwa na Manchester City yenye pointi 74 ikiwa imecheza mchezo mmoja pungufu, huku Arsenal ikikamata nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 35.

Liverpool inapewa nafasi ya kushinda mtanange huo, kutokana na kikosi cha Chelsea kuwa na majeruhi ambao wanategemewa akiwemo mlinda mlango Petr Cech na John Terry. Pia Chelsea itakosa huduma ya Ramires ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Mchezo wa Jumapili ambao Liverpool ndio wenyeji ni muhimu sana kwa Chelsea kushinda ili kujenga matumaini ya kutwaa kombe hilo. Vinginevyo nafasi hiyo itakwenda kwa Manachester City kuwania ubingwa na Liverpool.

Ushindi kwa Liverpool kutakoleza shamrashamra za kujiandaa kutwaa kombe hilo baada ya kulisotea kwa zaidi ya miongo miwili bila mafanikio.

Kazi imebaki kwa mameneja wa vilabu hivyo Brendan Rodgers na Jose Mourinho wote wawili wakihitaji ushindi ili kujiimarisha katika safari ya kulisaka kombe la ligi kuu England.