ManCity wanukia ubingwa England

Image caption Man City wanaelekea kileleni mwa ubingwa wa ligi ya Uingereza

Ilitarajiwa kwamba Manchester City itapiga hatua, lakini kwa mabao 4 - 0 dhidi ya Aston Villa, ilikuwa kweli mavuno yaliyowarejesha watakapo - kileleni na kuelekea ushindi wa dhahiri wa ligi ya England.

Yaya Toure ndiye aliyegonga bao hilo la mwisho, mengine wameyafunga kina Edin Dzeko mabao mawili na Stevan Jovetic bao moja.

Wakiwa na pointi 83 Man City wamewashinda Liverpool kwa pointi mbili na wingi wa mabao.

Wanachohitaji sasa ni pointi moja tu watakapokutana na West Ham hapo Jumapili ilhali Liverpool itakutana na Newcastle wakijua vyema kuwa matumaini yao ya kumaliza ukame wa kutwaa kombe hilo wa tangu miaka 24 iliyopita sasa yamefifia labda kutokee miujiza ya Man City wapoteze na wao washinde ndio waibuke na pointi 84.

Katika mechi nyengine Sunderland iliyokuwa mwanzoni inatishiwa kuteremshwa daraja wamenusurika kwa kuichapa West Brom 2-0.

Kwa matokeo hayo imeisukuma Norwich chini ya daraja, ambako imeungana na timu za Fulham na Cardiff katika safari ya kushuka daraja.