Onyo kuhusu mkanyagano DRC

Image caption Watu 15 wamefariki kufuatia mkanyagano uwanjani DRC

Kumekuwa na shutuma kali dhidi ya mamlaka ya kandanda katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo kuhusu msongamano wa watu uliotokea uwanjani wakati wa mechi ya soka Jumapili. Msongamano huo ulisababisha vifo vya watu 15.

Mwanahabari bingwa wa spoti Kabulo Muana Kabulo ambaye pia ni mkuu kitengo cha michezo katika idhaa ya taifa, ameiambia BBC kwamba mechi hiyo ilichezewa katika uwanja usiofaa, na kwamba uwanja haungeweza kuhimili idadi kubwa ya mashabiki waliofika kwa mchuano huo.

Aliongeza kwamba mashabiki wa timu moja walianza kuchocheza vurugu kabla ya mechi kuanza na kwamba alikuwa amewaonya maafisa wakuu kuhusu hatari ya kuruhusu mechi hiyo kuchezwa.

Inaripotiwa kuwa vita vilizuka kati ya mashabiki na mkanyagano ukazuka pale polisi walipowafyatulia mashabiki gesi ya kutoa machozi kuajribu kutuliza hali.