Kenya na Tanzania zaambulia patupu

Kenya na Tanzania zimeshindwa kufanya vizuri katika michuano ya kufuzu kombe la taifa bingwa Afrika mwaka 2015 huku Uganda ikifanikiwa katika hatua ya Makundi

Lesotho ilitoka sare ya kutofungana na Kenya mwishoni mwa juma jijini Nairobi, matokeo yaliyofanya Lesotho isonge mbele kwa ushindi wa goli la kufunga na kufungwa.

Kutokana na kupoteza mchezo huo, Shirikisho la Soka nchini Kenya limefuta kazi kitengo cha ufundi cha Harambee Stars , ikiwemo kumsimamisha kazi Kocha Mbelgiji Adel Amrouche.

Kikosi cha Harambee Stars kilikua chini ya usimamizi wa James Nandwa siku ya jumapili lakini naye alisimamishwa kazi sambamba na wahusika wa idara ya ufundi.

Mchezo huo uliisha kwa kutofungana ingawa Kenya ilitawala mchezo wakianza na Victor Wanyama anayoichezea Southampton na Mc Donald Mariga anayechezea ligi ya Italia

Kenya haikupata upenyo kufuta bao la Bushi Moletsane lililopigwa mjini Maseru wiki mbili zilizopita.

Mambo hayakua mabaya kwa Uganda ambayo iliifunga Mauritania 1-0.

Mauritania waliokuwa wenyeji wa mchezo huo walicheza wakiwa Kumi katika kipindi cha dakika kumi za mwisho baada ya kuondolewa kwa Karamoko Traore.

Robert Ssentongo alitupia goli pekee la dakika za majeruhi

Uganda itacheza na waliofuzu kundi E ambalo limekutanisha Ghana, Guinea na Togo.

Msumbiji ilivuka hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania na kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-3.

Mshambuliaji wa TP Mazembe Mbwana Samatta ailiipa matumani Tanzania kwa shambulio katika kipindi cha pili cha mchezo lakini Elias Domingues Pelelmbe aliipa ushindi Msumbiji.

Mozambique imefuzu kundi F, linalokutanisha Cape Verde, Niger na Zambia.

Mataifa 28 watakuwa katika makundi saba kucheza mwezi Septemba, Oktoba na Novemba ambapo michuano hiyo itaamua timu gani itaingia kwenye michuano ya kombe la mataifa Afrika mwaka 2015 nchini Morocco.