Setif,TP Mazembe watinga nusu fainali

Image caption Setif imejiunga na Mazembe katika kufuzu nusu fainali

Timu ya Algeria, Entente Setif, imefuzu kwa michuano ya nusu fainali kombe la klabu bingwa Afrika baada ya kwenda sare ya mabao mawili dhidi ya Esperance.

Matokeo hayo, yana maana kwamba Esperance ya Tunisia na bingwa mara mbili mwaka 1994 na 2011, walikosa kufuzu kwa nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010.

Setif ilijiunga na klabu nyingine ya Tunisia CS Sfaxien katika nusu fainali katika kundi B pamoja na TP Mazembe ya DRC ambao walifuzu katika kundi A baada ya kushinda Hilal ya Sudan kwa mabao 3-1.

Setif, ambao walikuwa mabingwa wa Afrika mwaka 1988, walifahamu kuwa kwenda sare nyingine nyumbani, ilitosha kwao kufuzu wakiwa wamesalia na mechi moja kucheza.

Akram Djahnit aliingiza mabao mawili ya Setif yaliyo wawezesha klabu hiyo kusonga mbele kwa kupata pointi waliyoihitaji mno.

Setif inashikilia nafasi ya pili katika kundi B kwa alama 9, alama moja nyuma ya CS Sfaxien waliopata nafasi hiyo mnamo siku ya Ijumaa baada ya kushinda Al Ahli Benghazi ya Libya kwa bao moja bila.