Barcelona yafungua msimu kwa ushindi

Image caption Barca imefungua msimu kwa ushindi mkubwa dhidi ya Elche

Lionel Messi alifunga mabao mawili na kuisaidia Barcelona kuilaza Elche mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya mkufunzi mpya Luis Enrique .

Barca wangesajili ushindi mkubwa zaidi ila tu mchezaji mpya Munir aligonga mwamba sawa na Andres Iniesta.

Lionel Messi hakukosea alipofungia Barca bao la kwanza kunako dakika ya 42 chini kwa chini na kumpa kocha mpya Enrique sababu ya kutabasamu katika mechi yake ya kwanza akiwa kocha.

Sekunde chache baadaye Javier Mascherano alitimuliwa uwanjani baada ya kumchezea visivyo Garry Rodrigues.

Barca ilienda mapumzikoni ikiwa kifua mbele na ilirejea ikiwa na hamu ya kutamatisha ushindi huo.

Mashambulizi yalianza moja kwa moja na Munir El Haddadi alifungia Barca bao la pili kunako dakika moja baada ya kipindi cha pili kuanza.

Kuanzia hapo haikuwa siri vijana wa Enrique walikuwa na niya ya kufungua ukurasa mpya msimu huu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kocha Enrique ameimarisha kikosi chake kwa niya ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Messi alifunga bao lake la pili na kuihakikishia Barca Ushindi huo wa kwanza msimu huu.

Kwa kocha Enrique ambaye alimrithi Tata Martino, ushindi huu ulikuwa dalili ya mambo kubadilika baada ya Tata kuiongoza Barcelona kwa msimu wake wa kwanza ambapo walikosa kushinda taji lolote tangu mwaka wa 2007-2008.

Enrique aliwasajili wachezaji wapya Luis Suarez kutoka Liverpool, Ivan Rakitic kutoka Sevilla na Thomas Vermaelen kutoka Arsenal ilikuimarisha nafasi zake za kutwaa ligi na hata kombe la mabingwa barani Ulaya.

Kocha huyo alikuwa hata na wasaa wa kuwashirikisha wachezaji wapya Rakitic, kipa Claudio Bravo, mlinzi Jeremy Mathieu washambulizi wachanga Munir na Rafinha ilikuwa na uhakika wa utendakazi wao uwanjani.