Nigeria yaponea marufuku ya FIFA

Image caption FIFA imesema haitaki tena mvutano huu la sivyo marufuku hiyo itawekwa

Fifa imethibitisha kuwa mabingwa wa Afrika Nigeria, wamefanikiwa kukwepa kupigwa marufuku kutoka kwa soka ya kimataifa.

Tisho la kuwapiga marufuku liliondolewa baada ya Aminu Maigari kuruhusiwa kuendelea kuwa Rais wa shirikisho la soka la Nigeria NFF.

Wadhifa wake, umekuwa ukizua malumbano kati yake na Chris Giwa, ambaye uchaguzi wake mwezi jana ulipuuzwa na Fifa.

Image caption Mashabiki wa timu ya taifa ya Nigeria Super Eagles

Hata hivyo Fifa imeonya kuwa changamoto zitakazoendelea kujitokea kuhusiana na uchaguzi huo huenda zikasababisha marufuku kuwekewa nchi hiyo.

Jukumu kuu la Maigari sasa ni kuandaa uchaguzi mpya kufanyika haraka iwezekanvyo kuwachagua wanachama wa NFF na wanachama wa bodi.

"tunawafahamisha kuwa ikiwa uchaguzi utaathirika kwa vyovyote, kesi hiyo itarejeshwa kwa Fifa tena na hili ni onyo kwa maafisa wa NFF, '' ilisema taarifa ya Fifa.

Kongamano litakalaofuata la Fifa litafanyika mwezi Mei mwaka 2015.