JS Kabylie yaadhabiwa kwa kifo cha Ebosse

Haki miliki ya picha
Image caption Kabylie hatacheza mechi za nyumbani hadi mwaka 2015

Klabu ya Algeria, JS Kabylie imepigwa marufuku kushiriki katika mechi za nyumbani hadi mwaka 2015 kufuatia kifo cha mchezaji wa Cameroon Albert Ebosse mwezi jana.

Mashabiki wa Kabylie pia wamepigwa marufuku kuhudhuria mechi zozote za nyumbani hadi mwanzoni mwa mwaka 2015.

Ebosse alifariki baada ya kugongwa na kombora tarehe 23 mwezi Agosti, baada ya JS Kabilye kushindwa na USM Alger kwa mabao mawili kwa moja katika mechi ya ligi.

Marufuku hiyo imetolewa na shirikisho la soka ya kulipwa ya Algeria.

Kabylie itaweza tu kushiriki mechi za nyumbani katika sehemu iliyotengwa hadi mwishoni mwa Februari.

Mashabiki wataruhusiwa tu kushiriki mechi ambazo hazitachezewa nyumbani bali ugenini mwezi Januari.

Mechi za ligi zitaanza kuchezwa siku ya Ijumaa jioni kwa mara ya kwanza tangu kifo cha Ebosse kutokea na mechi za mkondo wa tatu huku Kabylie akicheza Jumamosi.

Katika mkutano tofauti, maafisa wa shirikisho la soka la Algeria, walikutana na maafisa wa shriikisho la soka ya kulipwa, kujadili swala la kuongezeka kwa ghasia katika viwanja vya soka.