Liverpool yaua , Arsenal yachapwa Uefa

Haki miliki ya picha BBC World Service

Mashindano ya kutafuta klabu bingwa ya bara la ulaya katika mchezo wa soka ilianza jana huku timu kadhaa zikishuka katika viwanja mbalimbali ili kuanza kuzitafuta point tatu muhimu.

Mabingwa watetezi Real Madrid iliialika FC Basel katika uwanja wa Benabeu na kuanza vyema mbio za kutetea taji hilo kwa kuwafunga wapinzani wao kwa jumla ya mabao 5-1 huku washambuliaji wake wote wakiweza kuzifumania nyavu za wapinzani wao.

Katika viwanja vingine Liverpool imeutumia vyema uwanja wake wa nyumbani na kuibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Ludogorets Razgrad na kushuhudia mwanzo mzuri wa mshambuliaji Baloteli aliyefunga moja ya mabao hayo mawili.

Wenyeji Olympiakos ikaibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Atletico Madrid, huku timu ya Benfica ikizamishwa na wageni wao Zenit St. Petersburg kwa mabao 2-0, wakati Monaco ikishinda bao 1-0 dhidi ya Bayer Liverkusen. Dortimund ikashinda mabao 2-0 dhidi ya Arsenal na Galatasary ikatoka sare ya 1-1 dhidi ya Anderlecht.

Ligi hiyo inaendelea leo hii wakati Chelsea itacheza nyumbani dhidi ya FC Schalke 04, Bayern Munich dhidi ya Manchester city, AS Roma dhidi ya CSKA Moscow, Ajax dhidi ya PSG, Barcelona dhidi ya Apoel FC, NK Mariborv dhidi ya Sporting Lisbon wakati Athletic Bilbao dhidi ya Shakta Donestik na FC Porto itacheza na BATE.