Cameroon ni mwenyeji wa AFCON 2019

Cameroon  kuandaa AFCON 2019
Maelezo ya picha,

Cameroon kuandaa AFCON 2019

Cameroon ndiyo mwenyeji wa makala ya 2019 ya mashindano ya kuwania ubingwa wa Afrika.

Shirikiso la soka barani Afrika limeikabidhi Cameroon, jukumu hilo katika kikao cha kamati kuu ya CAF kilichofanyika mjini Addis Ababa Ethiopia.

Kamati hiyo iliamua pia kuipa Ivory Coast wajibu wa kuandaa makala ya mwaka wa 2021.

Hata hivyo CAF ilitangaza kuwa Guinea ndiyo itakayokuwa mwenyeji wa makala ya 2023 kinyume na matarajio ya wengi.

CAF iliamua kuwatunuku Guinea uwenyeji wa mashindano hayo kabla ya kukamilika kwa muda uliowekwa kwani Guinea ilikuwa imeonesha ari na hamu ya kuandaa makala hayo jambo ambalo liliisaidia kuzipiku Algeria na Zambia ambazo zilikuwa zinawania uwenyeji huo.

Cameroon, itakuwa inaandaa makala hayo kwa mara ya pili baada ya kuwa mwenyeji wa makala ya 1972 ya mashindano hayo ya Afrika.

Kulingana na taarifa ya CAF ,Cameroon,inalenga kutumia viwanja vya Bafoussam, Douala, Garoua na Yaounde kufanikisha awamu hiyo ya mashindano.

Furaha hiyo ya kutuzwa kuwa wenyeji wa mashindano ya kuwania ubingwa wa Afrika ilitanda hadi Ivory Coast, ambayo imeratibiwa kuandaa makala ya mwaka wa 2021.

Hii vilevile itakuwa mara ya pili kwa taifa hilo kuwa mwenyeji wa mchuano huo baada ya kuandaa kipute cha mwaka wa 1984.

Ivory Coast imeratibu kuandaa mashindano hayo katika miji ya Abidjan, Bouake, Korhogo, San Pedro na mji mkuu wa Yamoussoukro.

Maelezo ya picha,

AFCON :Ivory Coast kuandaa 2021,Guinea 2013

Guinea haijawahi kuandaa mashindano haya katika historia yake ya miaka 57.

Makala ya kwanza ya kombe la mataifa bingwa Afrika yaliandaliwa katika mji mkuu wa Sudan Khartoum.

Katika ombi lao kamati andalizi ya Guinea inapanga kuandaa mashindano hayo katika miji ya Conakry, Kankan, Labe na Nzerekore .

Sadfa ni kwamba CAF imeipiga marufuku Guinea kutoandaa mashindano yeyote kwani taifa hilo limeathirika na mlipuko wa Ebola.

Zambia licha ya kuwa ilishindwa ilikuwa imepanga kuandaa mashindano hayo katika ukanda wa ziwa Victoria.

Hiyo ndiyo mara ya pili kwa Zambia kupoteza nafasi ya kuandaa mashindano ya Afrika baada ya kupokonywa uwenyeji wa mwaka wa 1988 iliposhindwa kuthibitisha uwezo wake kwa wakati ufaao.

Makala ya mwaka huo yaliandaliwa na Morocco.

Kwa upande wao Algeria walitongewa na kifo cha mshambulizi wa JS Kabylie kutoka Cameroon Albert Ebosse baada ya kugongwa na jiwe akiwa uwanjani .

Kenya, Algeria, Ethiopia, Ghana, Mali na Zimbabwe zinawania kuandaa makala ya 2017 baada ya Libya kujiondoa kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama nchini humo.

Tarehe ya mwisho ya kupokea maombi ni Septemba 30.