Nigeria: Kura za NFF kufanywa Septemba 30

Fifa ilikuwa imetishia kuipiga marufuku Nigeria iwapo Maigiri angenyimwa fursa ya kuandaa uchaguzi mkuu
Maelezo ya picha,

Fifa ilikuwa imetishia kuipiga marufuku Nigeria iwapo Maigiri angenyimwa fursa ya kuandaa uchaguzi mkuu

Shirikisho la kandanda la Nigeria (NFF) limetangaza kwamba litafanya uchaguzi wake mnamo tarehe 30 septemba mwaka huu.

Tangazo hilo lilitolewa wakati wa mkutano wa kamati kuu ya NFF uliofanyika hapo jumamosi katika eneo la Warri ukiongozwa na rais wake anayeondoka Aminu Maigari.

Kamati ya uchaguzi na kamati ya rufaa ya uchaguzi zilibuniwa kama ilivyoagizwa na shirikisho la kandanda ulimwenguni (FIFA).

Kinyang’anyiro cha wadhifa wa Urais wa shirikisho la kandanda la NFF ni kati ya Amanze Uchegbulam, Taiwo Ogunjobi, Mike Umeh, Dominic, Shehu Dikko, Amaju Pinnick na Abba Yola.

Msemaji wa NFF Ademola Olajire ameiambia BBC michezo kwamba mkutano huo ulifuata maelekezo ya Fifa yaliyoagiza kwamba mkutano wa uchaguzi utahusisha wajumbe ambao walihudhuria mkutano wa mwisho wa mwaka uliopita uliofanyika Novemba katika mji wa Warri.

Wajumbe hao walikubaliana kwamba mchakato wa uchaguzi wenye uwazi na wa kuaminika lazima uwepo.

Uchaguzi huo ulikuwa umeratibiwa kufanyika tarehe 26 Agosti lakini ukaahirishwa kufuatia tofauti yaliyotokea wakati wa utayarishaji wa uchaguzi huo.

Matatizo hayo yaliongezeka pale Maigiri alipotiwa mbaroni huku Chris Giwa akichaguliza kuwa rais wa NFF kwa njia isiyoeleweka na kundi moja lililoungwa mkono na wizara ya michezo.

Maelezo ya picha,

Hatimaye Maigiri aitisha uchguzi tarehe 30 Septemba

Hata hivyo FIFA, lilitupilia mbali matokeo hayo na kutishia kuipiga marufuku nchi hiyo kushiriki kadanda ya kimataifa ikiwa Giwa hangejiondoa mamlakani kufikia tarehe mosi septemba na kumrudisha Maigari na wafanyakazi wake mamlakani.

Tishio hilo la marufuku liliondolea wakati Maigari aliporudishwa madarakani kama rais wa NFF.

Aidha mwenyekiti huyo aliyekumbwa na malumbano ya uongozi na tuhuma za utumizi mbaya wa mamlaka akapatiwa mamlaka ya kupanga uchaguzi mwingine haraka iwezekanavyo.