Uganda haitaanda mashindano ya Kriketi

Mashindano hayo sasa yatafanyika nchini Malaysia
Maelezo ya picha,

Mashindano hayo sasa yatafanyika nchini Malaysia

Uganda imevuliwa uwezo wa kuandaa mashindano ya kimataifa ya kriketi divisheni ya tatu kutokana na hofu ya usalama nchini humo.

Mashindano hayo, ambayo yanajumuisha timu ya Marekani, yalipaswa kuandaliwa kati ya tarehe 26 Oktoba na tarehe 2 Novemba.

Baraza la kimataifa la Kriketi ICC, limesema kinyang'aniro hicho sasa kitafanyika mjini Kuala Lumpur, Malaysia.

Mapema mwezi huu, polisi nchini Uganda walisema kuwa walinasa vilipuzi kutoka kwa watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kiisilamu.

Maafisa wa utawala walisema kwamba washukiwa wa kundi la Al Shabaab walikuwa wanapanga kufanya mashambulizi katika mji mkuu wa Uganda,Kampala.

Msako wa polisi ulifanyika baada ya onyo kutoka kwa ubalozi wa Marekani kwamba mashambulizi ya kigaidi ya kulipiza kisasi huenda yakafanywa mjini Kampala dhidi ya masilahi ya Marekani.

Yangekuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi mauaji ya kiongozi wa kundi hilo,Ahmed Abdi Godane.

Wanajeshi wa Uganda wako kwenye kikosi cha muungano wa Afrika, kinachokabiliana na wanamgambo wa Al Shabaab nchini Somalia.

Wapiganaji wa kundi hilo ndio waliofanya mashambulizi mawili na kuwaua mashabiki 76 wa soka waliokuwa wanatazama michuano ya fainali ya kombe la dunia mwaka 2010.