Bayern yashinda,Barcelona hoi UEFA

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bayern Munich

Kitimtim cha klabu bingwa barani Ulaya kiliendelea tena usiku wa kuamkia leo huku zikishuhudiwa nyasi za viwanja kadhaa zikiwaka moto kuruhusu wababe wa soka kutoka nchi mbalimbali wakizitafuta point tatu muhimu.

Nchini Ufaransa wenyeji Paris St Germany (PSG), waliikaribisha timu ya Barcelona, hadi mwisho wa mchezo huo wenyeji PSG wakaibuka washindi kwa jumla ya mabao 3-2.

Nchini Urusi wenyeji CSKA MOSCOW wameangukia pua baada ya kufungwa goli 1-0 na wababe wa soka wa Ujerumani Bayern Munich, goli lililofungwa kwa njia ya penalty na mshambuliaji Thomas Muller lilitosha kuwapa ushindi vijana hao wa Pep Guadiola.

Nayo Manchester City walikuwa wenyeji dhidi ya AC Roma katika uwanja wa Etihad, hadi mwisho wa mchezo timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1, huku waingereza wenzao Chelsea wakikusanya point zote tatu katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Sporting Lisbon ya Ureno mfungaji wa goli akiwa ni Nemanja Matic.

Kwingineko Schalk 04 ilitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya NK Maribor ya Slovania, BATE Borisov ya Belarus ikaichapa Athletic Bilbao wa jumla ya mabao 2-1, nao Ajax wakatoka sare ya 1-1 dhidi ya Apoe Nicosia ya nchini Cyprus

Ligi hiyo itaendelea tena usiku wa leo huku timu kadhaa zikitarajia kushuka dimbani.

Liverpool itakuwa mgeni wa FC Basel ya Uswiz, Arsenal itavaana na Galatasaray ya Uturuki, Atletico Madrid itawakaribisha Juventus ya Italy, Malmo FF ya Sweden itamenyana na Olympiakos ya Ugiriki, wakati mabingwa watetezi Real Madrid watakuwa wageni wa Ludogorets Razgrad ya Bulgaria, Zenit St. Petersburg ya Urusi itawakaribisha Monaco ya Ufaransa huku Bayer liverkusen itakuwa nyumbani kucheza na Benfica, nayo Anderlecht ya Ubeligiji itavaana na Borusia dotmund ya Ujerumani