Mwenyekiti mpya wa soka atajwa Nigeria

Image caption Mwenyekiti mpya wa shirikisho la Soka nchini Nigeria NFF Pinnick Amaju

Shirikisho la soka nchini Nigeria NFF limemchagua Amaju Pinnick kama rais wake mpya baada ya kufanyika kwa uchaguzi siku ya jumanne.

Pinnick Mwenye umri wa miaka 43,ambaye ni mwenyekiti wa tume ya michezo ya Delta state,afisa mkuu wa Delta FA na mwenyekiti wa Warri Wolves alipata kura 32 kati ya 44 zilizokuwepo katika raundi ya pili ya uchaguzi huo.

Wapinzani wake Dominic Iorfa na Taiwo Ogunjobi walijipatia kura nane na nne mtawalia.

Hatahivyo,mgombea aliyedaiwa kuwa kifua mbele katika kazi hiyo Shehu Dikko alisalimu amri.

Matatizo kadhaa yalijitokeza wakati wa maandalizi ya kura hiyo baada ya afisa mkuu anayesimamia uchaguzi Samson Ebomhe kukamatwa na maafisa wa kitengo cha ujasusi nchini Nigeria DSS,kabla ya kuwachiliwa baadaye ili kusimamia uchaguzi huo.

Uchaguzi huo unamaanisha kuwa taifa la Nigeria sasa litaepuka vikwazo vikali.

Iwapo uchaguzi huo usingefanyika ,Nigeria ingepigwa marufuku katika soka ya kimataifa hadi mkutano mwengine wa shirikisho la soka duniani FIFA mnamo mwezi May 2015.

Upinzani mkali katika uchaguzi huo ulikuwa kati ya Amanze Uchegbulam ,Taiwo Ogunjobi ,Mike Umeh,Dominic Iorfa pamoja na Shehu Dikko,Amaju Pinnick na Abba Yola.