Elmohamady ajiondoa katika timu ya Misri

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ahmed Elmohamady kulia

Mchezaji wa timu ya Hull City nchini Uingereza Ahmed Elmohamady amejiondoa katika kikosi cha Misri kitakachokabiliana na timu ya Botswana katika mechi mbili za kufuzu katika kombe la taifa bingwa barani Afrika mwezi huu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alijeruhiwa wakati timu hiyo ilipopata ushindi katika mechi dhidi ya Crystal Palace siku ya jumamosi.

Timu ya Hull imesema kuwa mchezaji huyo anauguza jeraha la mgongo.

Misri itachuana na Botswana ugenini siku ya ijumaa na baadaye katika uwanja wa nyumbani siku tano baadaye huku shinikizo zikizidi dhidi ya Kocha Shawky Gharib baada ya timu hiyo kushindwa mara mbili katika kundi la G.

Timu hiyo ya Pharaoh haina pointi hata moja ,pamoja na timu ya Botswana na sasa inakabiliwa na kibarua kigumu kufuzu katika mechi za kombe la taifa bingwa barani Afrika nchini Morrocco.

Siku ya jumanne Rais wa shrikisho la soka nchini Misri Gamal Allam alisema kuwa kushindwa kwa timu hiyo ya taifa ni jukumu la kamati yake ya kiufundi.

''Tutamuajiri meneja kutoka nchi za kigeni iwapo Gharib atashindwa kuipeleka timu hiyo katika mashindano ya taifa bingwa barani Afrika'',alisema Gamal.