Manchester City wakubali kipigo kwa CSKA

Haki miliki ya picha AP
Image caption Manchester vs CSKA

Safari ya Manchester City kutwaa ubingwa wa ligi ya mabingwa barani Ulaya imeingia mikosi zaidi baada usiku wa kuamkia leo kukubali kugaragazwa nyumbani Etihad na Warusi wa CSKA Moscow na kuufanya kuwa usiku mbaya jijini Manchester.

Licha ya kuruhusu mabao mawili ya kipindi cha kwanza yaliyotiwa wavuni na Seydou Doumbia pia viungo wake muhimu Yaya Toure na Fernandinho walitolewa nje kwa kadi nyekundu na hivyo wataikosa mechi ngumu ijayo dhidi ya Bayern Munich. Yaya Toure alisawazisha bao la kwanza la Doumbia lakini haikusaidia kitu kwani mchezo wa chini ya kiwango unaoikabili timu hiyo hivi karibuni umeigharimu katika kundi lake kiasi cha kucheza mechi nne na kupata pointi mbili tu. City haijashinda hata mechi moja na sasa wanapaswa kuzifunga Munich na Roma katika michezo iliyosalia ili kupata njia ya kusonga mbele hatua ya 16 bora.

Yaya Toure amewaomba radhi mashabiki na wapenzi wa timu yake kwa kupewa kadi nyekundu kwa mara ya kwanza akiichezea Man City. Mechi zingine za ligi hiyo zilizopigwa jana usiku ni pamoja na ile ya Bayern Munich iliyoifumua AS Roma 2-0 mjini Munich, Ajax Amsterdam ikiwa nyumbani imesagwa 2-0 na Barcelona, huku NK Mariobor wakiibana mbavu Chelsea kwa kufangana 1-1.

Shaktar Donetsk imeivurumisha BATE Borisov mabao 5-0 ilhali Paris Saint Germain imepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 mbele ya Apoel Nicosia. Mechi zinazofuata zitachezwa Novemba 25.