Wachezaji wa Spurs wahofia kuzomewa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Adebayor anasema anahofia wachezaji kuzomewa hali inayowatoa motisha

Mchezaji soka wa klabu ya Tottenham Emmanuel Adebayor, amesema kuwa wachezaji wa klabu hiyo wanaogopa kuchezea katika uwanja wao wa nyumbani.

Hii ni kutokana na kejeli zinazotolewa na mashabiki wa klabu hiyo kwa wachezaji katika uwanja wao wa nyumbani White Hart Lane, hali ambayo Adebayor anasema inaathiri wachezaji kimawazo.

Wachezaji hao walizomewa na mashabiki wao baada ya kushindwa nyumbani na Stoke Jumapili kwa mabao 2-0.

Tayari wameshindwa mechi nne kati ya sita walizochezea katika uwanja wao wa White Hart Lane msimu huu.

"kwa sasa mimi naona itakuwa vyema kucheza katika uwanja mwingine kule nje,'' alisema Adebayor.

"hivyo itakuwa vyema maana kama ni kuzomewa tutazomewa na mahasimu wala sio mashabiki wetu. ''

Spurs, waliocharazwa na Newcastle katika mechi yao iliyopita, wamepata tu alama sita katika mechi walizocheza nyumbani.

Naye mkuu wa klabu hio amewataka mashabiki kubadili mawazo kuhusu klabu yao.

Adebayor aliongeza kusema itakuwa vyema kucheza ugenini sio kwa ajili yake tu bali hata kwa wachezaji wengine kwani watakwepa kuzomewa na mashabiki.

Adebayor amecheza mechi 11 za kwanza za Tottenham msimu huu huku akiingiza mabao kadhaa katika mechi dhidi ya QPR na nyingine waliyocheza dhidi ya Newsastle oktoba 26.