Morocco yakataa kuandaa CAF 2015

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ebola ndio imezua hofu kiasi cha Morocco kusita kuandaa Caf 2015

Morocco haitakuwa mwenyeji wa dimba la kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2015, kwa sababu ya hofu ya kuenea kwa ugonjwa wa Ebola.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa shirikisho la soka Afrika Caf.

Hata hivyo, Caf haijatangaza eneo ambako michuano hiyo itafanyika kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 8 mwezi Februari.

Shirikisho hilo limesema tarayari lina maombi kutoka kwa baadhi ya mashirika ya kitaifa yanayotaka kupewa nafasi ya kuandaa michuano hiyo.

Shirikisho la Caf lilitimua Morocco kutoka fainali ya michuano hiyo, wakati ikiwa imejiandaa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Morocco ilikuwa imepewa hadi Jumamosi kufanya uamuzi ikiwa itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo au la.

Ilikuwa imeomba kuahirisha michuano hiyo hadi mwaka 2016.

Kamati kuu ya CAF ilikutana mjini Cairo Jumanne na kuthibitisha kuwa ilipata maombi kutoka kwa mataifa mengine kuandaa michuano hio.

Shirikisho hilo linatathmini maombi hayo na kwamba litafanya uamuzi hivi karibuni.

Mechi za kufuzu zitaendelea kama ilivyopangwa kufanyika tarehe 14 na 15 Novemba kuamua timu 15 zitakazojiunga na taifa litakalokuwa mwenyeji kwa mechi za fainali.

Watu 4,960 wamefariki kutokana na Ebola hasa katika mataifa ya Afrika Magharibi, hasa nchini Sierra Leone, Liberia na Guinea.

Morocco ilikuwa imeelezea wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya watu ambao wangeingia nchini humo, kwa michuano hio.