Podolski ataka kuihama Arsenal

Image caption Mchezaji wa Arsenal Lucas Podolski ataka kuihama kilabu hiyo ili kupata fursa za kuchezeshwa mara kwa mara.

Mchezaji huyo wa Ujerumani alilichezea taifa lake kwa dakika 90 dhidi ya Gibraltar siku ya ijumaa lakini anashangazwa kuona ni kwa nini hajaanzishwa kuichezea kilabu yake ya Arsenal.

Kulingana na mtandao wa Goal.com Lucas Podolski anasema kuwa mkufunzi wa kilabu hiyo Arsene Wenger anampuuza.

Mshambuliaji huyo amechezeshwa mechi nne pekee katika ligi ya Uingereza msimu huu,huku akianzishwa katika mechi ya kombe la Carling ambapo Arsenal ilipoteza kwa Southampton mnamo mwezi Septemba.

Lucas Podolski alicheza dakika 90 wakati Ujerumani ilipoicharaza Gibraltar mabao 4-0 katika mechi za kuwania kufuzu katika dimba la Ulaya,lakini mkufunzi Joachim Low anataka mchezaji huyo kuanza kuchezeshwa mara kwa mara katika kilabu yake.

Mchezaji huyo aliyetoka kilabu ya Koln nchini Ujerumani alisema kwamba anapanga kufanya mazungumzo na Arsenal kuhusu hatma yake mwezi january na akasisitiza tena siku ya ijumaa wakati taifa lake liliposhinda.

''Nimekuwa nikiichezea Arsenal kwa dakika chache ,niko tayari kuionyesha Arsenal kile naweza kuifanyia ,lakini fursa hiyo haipatikani'',alisema Podolski.