Ghana yapoteza kesi dhidi ya marufuku

Image caption Timu ya wachezaji wasio zidi miaka 17 nchini Ghana

Ghana imepoteza kesi yake ya rufaa dhidi ya marufuku iliowekewa timu yake kushiriki katika dimba la wachezaji wasiozidi miaka 17 mwaka ujao.

Shrikisho la soka barani Afrika liliipiga marufuku Ghana kwa kumuorodhesha mchezaji aliye na umri wa juu Issac Twum dhidi ya Cameroon katika mechi ya kufuzu.

Ghana ilishinda mechi yake ya Kwanza kwa mabao 2-1 na baadaye kupata ushindi wa mabao 6-4 kwa jumla.

Lakini Cameroon ilipinga matokeo hayo na hivyobasi Shirikisho la CAF likaamua kumpiga marufuku Twum.

Shirikisho hilo lilifichua kuwa mchezaji huyo ambaye aliwahi kuiwakilisha timu yake ya vijana ya Kpando Heart Lions alifeli mahitaji ya kushiriki katika mechi hizo baada ya kufanyiwa ukaguzi wa miaka yake.

Rufaa huenda ikawasilishwa dhidi ya uamuzi huo wa Caf katika mahakama ya usuluhishaji wa migogoro ya michezo katika kipindi cha siku 10 zijazo.

Kamati kuu ya shrikisho la soka nchini Ghana inakutana hii leo ili kutafuta hatua watakayochukua.