Pele aendelea kupata afueni hospitali

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Aliyekuwa nyota wa kikosi cha Brazil Pele

Mchezaji wa zamani wa timu ya Brazil Pele anendelea kupata afueni lakini bado amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi akiwa na maambukizi ya eneo la kupitisha mkojo mapema wiki hii.

Habari hizo zinajiri baada ya gwiji huyo wa soka kusema katika mtandao wa twitter kwamba anaendelea kupata afueni katika hospitali moja ya Albert Einstein iliopo mjini Sao Paulo.

Hatahivyo msaidizi wa mzee huyo mwenye umri wa miaka 74, Jose Fornos alipuuzilia mbali habari hizo.Lakini hospitali hiyo imesema kuwa Pele anaendelea kupata msaada wa muda wa figo yake na kwamba hahitaji usaidizi wowote wa kupumua.

Taarifa hiyo iliongezea kwamba mchezaji huyo wa zamani anaendelea kupata afueni na kwamba bado amesalia katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Pele

Awali Hospitali hiyo ilikuwa imesema kwamba Pele alikuwa amelazwa na akiwa hali mbaya.

Lakini baadaye Pele akaandika kwamba yu buheri wa afya katika mtandao wake wa Twitter na alikuwa amehamishwa hadi chumba maalum ndani ya hopsitali hiyo kutokana na maswala ya faragha.

Aliongezea kwamba ijapokuwa anawashukuru wale wote waliomtembelea kumpa pole ,alitaka kuendelea na matibabu yake kwa njia ya amani.

Amesema kwamba angependa kuwa na familia yake wakati wa sikukuu na ataanza mwaka mpya akiwa katika afya nzuri huku ziara nyingi za kimataifa zikiwa tayari zimepangwa.