Ushabiki wa soka wamtia matatani mwanamke

Image caption Wanawake wanaruhusiwa kucheza soka lakini hawaruhusiwi kukaa sehemu moja na wanaume

Mchezaji na shabiki sugu wa soka mwanamke nchini Saudi Arabia, amejipata mashakani baada ya kuingia katika uwanja uliokuwa na mashabiki wanaume.

Viwanja vya soka nchini humo vina masharti yake , kwani wanawake na wanaume hawaruhusiwi kuchanganyikana.

Kulingana na taarifa za vyombo vya habari, shabiki huyo mwanamke aliingia uwanjani akiwa amevalia kama mwanamume.

Aliingia uwanjani akiwa amevalia kofia kubwa iliyokuwa imefungwa na kitambaa cheusi cha kujitanda kichwani pamoja na mavazi meupe ya timu iliyokuwa inacheza ugenini.

Alikaa mbali na mashabiki wengine wanaume akiwa peke yake kazingirwa tu na viti.

Lakini hapo ndipo unga ulizidi maji kwani aliweza kutambuliwa

Polisi walimkamata na kusema kuwa watampeleka kwa maafisa wakuu.

Lakini raha aliyoipata shabiki huyo sugu licha ya masaibu yake ni kwamba klabu aliyokuwa anashabikia iliibuka na ushindi.