Wanariadha wakenya wapigwa marufuku

Haki miliki ya picha b
Image caption Rita Jeptoo mwanariadha mashuhuri wa Kenya alipatikana na hatia ya kutumia dawa haramu mbioni

Wanariadha wawili wa Kenya Viola Chelangat Kimetto na Joyce Jemutai Kiplimo, wamepataikana na hatia ya kutumia dawa haramu za kusisimua misuli.

Wanariadha hao sasa wamepigwa marufuku kwa miaka miwili.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa shirikisho la riadha nchini humo.

Wanariadha hao wawili wanawake, walipatikana na hatia ya kutumia dawa aina ya Norandrosterone.

Kimetto alipatikana na hatia hio Disemba mwaka 2013, huku Kiplimo akipatikana na kosa hilo baada ya kushiriki mbio za masafa marefu mjini Yangzhou China Aprili.

Shirikisho la riadha la Kenya linasema linachunguza wanariadha wengine watano wanaoshukiwa kutumia dawa hizo haramu.

Kadhalika shirikisho hilo limesema kuwa wanariadha hao wametakiwa kufika katika ofisi zake siku ya Alhamisi kuzungumzia maswala kadhaa kuhusiana na utumiaji wa dawa zilizopigwa marufuku, ambazo zimetajwa na shirikisho hilo.

Kimetto na Kiplimo ni wanariadha wa hivi karibuni kupatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli, kati ya wanariadha wengine 40 katika kipindi cha miaka miwili.

Bingwa wa Olimpiki, David Rudisha alisema wiki jana kwamba serikali haifanyi juhudi za kutosha kukabiliana na tatizo la utumiaji wa dawa haramu za kusisimua misuli miongoni mwa wanariadha.

Onyo lake limetolewa takriban miaka miwili baada ya Moses Kiptanui, mmoja wa wanariadha mahiri nchini Kenya kupatikana na hatia ya kutumia dawa hizo.

Bingwa huyo wa dunia mara tatu wa mbio za mita 3,000 pamoja na mkufunzi, alidai kuwa wanariadha wengi wamekuwa wakitumia dawa haramu za kusisimua misuli ili kujipatia utajiri wa haraka.

Miezi miwili iliyopita,Rita Jeptoo,mshindi wa mbio za marathon za Boston na Chicago kwa miaka miwili iliyopita, aliibuka na kuwa wanariadha maarufu sana kupatikana akiwa ametumia dawa za kusisimua misuli.