FIFA sasa kuchapisha ripoti ya Garcia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Aliyekuwa mchunguzi wa kamati ya maadili katika shirikisho la soka FIFA.

Maafisa wakuu wa shirikisho la FIFA wamekubaliana kuchapisha ripoti yote kuhusu uchunguzi wa madai ya ufisadi uliotokea wakati wa kutolewa kwa kandarasi za kombe la dunia kwa mataifa ya Urusi mwaka 2018 na Qatar mwaka 2022.

Wamekubaliana kutoa kurasa 430 za uchunguzi wa Michael Garcia baada ya kufanya mkutano kufuatia pendekezo la mkuu wa kufuata maagizo Domenica Scala.

Ripoti hiyo itawekwa wazi baada ya uchunguzi unaondelea kuhusu watu watano kukamilika na inatarajiwa kufanyiwa uhariri ili kuficha majina ya mashahidi.

Hatua hiyo ya kuichapisha ripoti hiyo inaonyesha mabadiliko ya sera baada ya FIFA kukataa shinikizo kutoka kwa Garcia mwenyewe na wengine kutoa ripoti hiyo.

Garcia alijiuzulu siku ya Jumatano baada ya ombi lake la kupinga ripoti fupi ya uchunguzi wake iliotolewa na mwenyekiti wa kamati ya maadili katika shirikisho hilo Hans-Joachim Eckert kukataliwa.