"Siogopi kibarua kuota nyasi": Kocha wa Yanga

Image caption Kikosi cha watoto wa Jangwani Yanga

Kuna msemo maarufu usemao” Makocha wana ajiriwa ili wafukuzwe na usemi huo umejidhihirisha sehemu mbalimbali duniani na katika ligi maarufu barani Ulaya, Afrika na kwingineko.

Katika kile kinachoonekana kwa makocha wengi kuwa msemo huo upo kichwani pale tu wanapopata ajira, kocha Mholanzi, Hans Van Der Pluijm amesema yuko tayari kufukuzwa na mabingwa wa zamani wa Tanzania bara, Yanga endapo wataamua kufanya hivyo kabla ya mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu kuisha.

Akizungumza baada ya kuonekana kwake rasmi katika makao makuu ya klabu hiyo, Pluijm amesema ataheshimu maamuzi hayo endapo yatatokea kama timu itafanya vibaya, lakini ameweka akiba kwa kusema kuwa hategemei hilo kutokea.

“Nina imani timu itafanya vizuri kitaifa na katika michuano ya kimataifa”.‘Lakini hili ni jukumu letu sote, kwa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki”, alisema mdachi huyo.

Yanga, inayokabiliwa na michuano ya vilabu ya shirikisho la mpira wa miguu Afrika (CAF), ni moja ya klabu kongwe nchini Tanzania (ilianzishwa mwaka 1930).

Hivi karibuni iliwatimua makocha kutoka Brazil, Marcio Maximo na msaidizi wake Leonardo Neiva (ndani ya miezi 3 tu) kwa kutoridhishwa na utendaji wao.

Yanga na watani wao wa jadi, Simba ni miongoni mwa vilabu vikubwa Afrika vikiwa na historia ya kufukuza makocha pindi matokeo yanapokuwa ndivyo sivyo, na hasa endapo mmoja wa makocha hao atafungwa mfululizo na hasimu wake au kupoteza ubingwa.

Imeripotiwa kuwa Yanga na Simba zimefukuza makocha tisa kwa kipindi cha miaka mitatu.Simba ndiyo inayoongoza kwa kuwatimua makocha watano wakati Yanga imefungisha virago makocha wanne kuanzia 2010 hadi 2013.

Makocha waliokumbwa na mkasa wa kutimuliwa kwa upande wa Simba ni Patrick Phiri (Zambia), Milovan Cirkovic (Serbia), Moses Basena (Uganda), Patrick Liewig (Ufaransa) na Mtanzania pekee Abdallah Kibadeni.

Yanga iliwatimua Sam Timbe (Uganda), Kostadin Papic (Serbia), Tom Saint Fiet (Ubelgiji) na Ernest Brandts kutoka Uholanzi