Baseball Tanzania yapata mhisani

Image caption Salama na umoja michezoni

Serikali ya Japan, kupitia baraza lake la michezo imeelezea nia yake ya kusaidia kukuza mchezo wa baseball nchini Tanzania.

Mchezo huo una miaka miwili tangu uanzishwe Tanzania na tayari viongozi wa mchezo huo wameonesha nia ya kushiriki michuano ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo mwaka 2020.

Katibu mkuu wa chama cha baseball, , Alpherio Nchimbi amesema wanaishukuru Japan kwa msaada wa kiufundi itakaoutoa katika kukuza mchezo huo na kuiwezesha timu kusafiri Kenya kucheza michuano ya kufuzu kombe la dunia, iliyomalizika hivi karibuni na Tanzania kushika nafasi ya tatu. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki michuano ya kimataifa kwa mchezo huo maarufu duniani na hasa Asia na Amerika.

Balozi wa Tanzania nchini Tanzania, Masaki Okada amesema baseball ni mchezo unaopendwa sana nchini Japan zaidi ya michezo yote.

“Nchi yangu imekuwa mabingwa wa dunia mara mbili”.

“Mwaka 2020, tutakuwa wenyeji wa Olimpiki na tunapiga debe ili baseball iweze kuwa miongoni mwa michezo itakayoshindaniwa”, alisema Okada. Tayari Japan imesaidia kufanyika kwa michuano ya pili ya Taifa iliyofanyika Dar es Salaam na kushirikisha timu za shule.

Japan, kupitia mradi wake wa “Sport for Tomorrow”, inasaidia zaidi ya nchi 100 duniani katika jitihada zake za kuitangaza michuano ya Olimpiki huko Tokyo na kueleza dunia utayari wake wa kuwa mwenyeji wa Olimpiki 2020.

Brazil, kupitia mji wake wa Rio de Janeiro, ndio itakuwa mwenyeji wa michuano ya mwaka 2016 itakayofuatiwa na ya Tokyo, miaka minne baadae.