Azam watamba kuifunga KCC ya Uganda

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Timu ya Azam

Mabingwa watetezi wa soka Tanzania bara, Azam FC wamepania kuwafunga KCC ya Uganda katika mechi ya ufunguzi ya kombe la Mapinduzi ya Zanzibar linakaloanza January 1 visiwani Zanzibar.

Kulikuwa na tetesi kuwa mabingwa hao wangeweza kukutana na wapinzani wao wa kombe la klabu bingwa Afrika, El-Merreikh ya Sudan, ambao waliombwa kuwa sehemu ya timu shiriki katika moja ya mechi ya michuano hiyo., Lakini mpaka hivi punde, taarifa zilisema kuwa El-Merreikh hawatashiriki kutokana na waandaaji kushindwa kukidhi baadhi ya mahitaji yao.

Iwapo mabingwa hao wa kombe la shirikisho la Afrika 2014/2015, El-Merreikh watashiriki, basi msisimko wa michuano hiyo utaongezeka.

“Tumejipanga vya kutosha na kuwa mabingwa”.

“Tuna taarifa kuwa El-Merreikh watashiriki, kama ni kweli itakuwa ni kipimo tosha baina yetu kabla ya kucheza hapo mwakani (kati ya Januari 13, 14 au 15) katika mechi za hatua za awali za michuano ya klabu bingwa Afrika”, alisema msemaji wa klabu ya Azam, Jaffar Iddi.

Timu za Yanga, Simba na Mtibwa sugar zitaungana na Azam kutoka Tanzania Bara kushiriki michuano hiyo yenye lengo la kuadhimisha Mapinduzi tukufu ya Zanzibar yaliyotokea mwaka 1964.

Timu wenyeji ni KMKM, Mafunzo, Mtende Rangers na Shaba wakati kulikuwa na taarifa kuwa Ulinzi ya Kenya nayo ilitegemewa kushiriki lakini haitasafiri kwenda Zanzibar.