Simba SC mabingwa wa kombe la mapinduzi

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Kikosi cha Mnyama-Simba

Timu ya Simba Sc imeibuka kidedea kwa kutwaa kombe la mapinduzi kwa mikwaju 4-3 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo ulipigwa kwenye dimba la Amaani Visiwani Zanzibar.

Dakika tisini za mchezo za kawaida zilimalizika kwa timu hizi kwenda sululu ya bila kufungana ndipo changamoto ya mikwaju ya penati ikafuata .

Penati za simba zilifugwa na Awadh Juma, Hassan Kessy, Hassan Isihaka na Dan Ssenrukuma wakati ya Shaaban Kisiga iliokolewa na Kipa Said Mohamed.

Penati za Mtibwa Sugar zilifungwa na Ally Lundenga, Shaaban Nditi na Ramadhan Kichuya huku Ibrahim Rajab ikigonga mwamba huku penati ya Vincent Barnabas ikiokolewa na kipa Ivo Mapunda.

Nahodha wa Simba, Hassan Isihaka,alikabidhiwa Kombe la Mapinduzi pamoja na Shilingi Milioni 10 kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta Ali Mohammed Shein.

Kipa Said Mohammed wa Mtibwa Sugar amekuwa kipa bora wa michuano,beki wa kati wa Mtibwa Sugar, Salim Mbonde ameibuka kuwa mchezaji bora wa michuano.Mfungaji bora amekuwa Simon Msuva wa Yanga ambaye alifunga mabao manne.