Tanzania:Azam Fc kuweka Kambi Dr Congo

Image caption Kikosi cha Klabu ya Azam

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Azam FC wanatarajiwa kuweka kambi nchini Jamhuri ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kucheza mechi nne za kirafiki ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na mechi ya awali ya kombe la klabu bingwa ya Afrika dhidi ya vigogo wa Sudan, El-Merreikh.

Msemaji wa klabu ya Azam, Jaffar Iddi amesema wakiwa Congo, watacheza na timu kubwa nne na kurejea nchini February 4 kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya kucheza na El-Merreikh Jijini Dar es Salaam kati ya February 13, 14 na 15.

“Bado hatujajua timu tutakazocheza nazo kwa kuwa bado tupo katika mazungumzo”, alisema Idd.

Azam, ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki klabu bingwa Afrika, itaondoka kwenda Kongo mapema baada ya machi yao ya ligi kuu Tanzania Bara itakayochezwa Januari 24 dhidi ya mabingwa wa zamani, Simba Sports Club.

Wakati Azam ikiwa katika maadalizi ya kucheza mechi za kirafiki za kimataifa, wapinzani wao, E-Merreikh tayari wamecheza mechi kadhaa za majaribio ikiwa ni pamoja kutoka droo ya 2-2 na Schalke O4 inayoshiriki ligi ya Bundesliga ya Ujerumani. Mechi hiyo ilicheza Aspire Academy mjini Doha, Qatar mapema mwaka huu.

Pia El-Merreikh wanategemewa kucheza na mabingwa wa Uganda, KCC mjini Khartoum, leo (Jumanne) usiku katika mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa katika maandalizi yao dhidi ya Azam.

Mechi ya marudio kati ya Azam na El-Merreikh itafanyika baada ya wiki mbili mjini Khartoum, Sudan.

Mbali na Azam, wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya CAF ya vilabu ni Young Africans (Yanga), wanaotegemewa kucheza na timu ya jeshi la Botswna, BDF XI katika mechi ya awali ya kombe la shirikisho.

Kwa upande wa Zanzibar, mabingwa KMKM watakiputa na timu nyingine ngumu ya Sudan, Al Hilal katika klabu bingwa Afrika wakati katika kombe la shirikisho, Polisi watacheza na CF Mounana ya Gabon.