AFCON:Kundi B limemenyana vikali

Kindumbwendumbwe cha michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kinaendelea nchini Equatorial Guinea ambapo mzunguko wa pili uliendelea jana kwa timu za kundi B kumenyana. Katika mchezo wa awali wa kundi hilo Tunisia iliinyuka Zambia mabao 2-1. Katika mchezo huo Zambia ndio waliokuwa wa kwanza kuziona nyavu za Tunisia katika dakika ya 59 likifungwa na Mayuka. Tunisia iliamka na kusawazisha katika dakika ya 70 kupitia kwa Akaichi na Chikhaoui akamaliza kazi katika dakika ya 88 kwa kukwamisha mpira langoni mwa Zambia. Kukosa umakini katika safu ya ushambuliaji na ulinzi kuliikosesha Zambia ushindi katika mchezo huo.

Katika mchezo wa pili wa kundi B, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Cape Verde zilitoka sare ya kutofungana huku kila timu ikishindwa kutumia nafasi ilizotengeneza kupata magoli. Kwa matokeo hayo Tunisia sasa inaongoza ikiwa na pointi nne, ikifuatiwa na timu za Cape Verde na DR Congo zenye pointi mbili kila moja na mkiani ni Zambia yenye pointi moja. Kabla ya michezo yao ya jana timu hizo zilikuwa na pointi moja kila moja.

Mzunguko wa pili utaendelea kwa timu za kundi C kupambana. Ghana itaumana na Algeria, ambapo Afrika Kusini itahenyeshana na Senegal katika mchezo wa pili wa kundi hilo. Katika mechi za kwanza kwa timu hizo, Algeria iliizamisha Afrika Kusini kwa mabao 3-1, huku Senegal ikiinyamazisha Ghana kwa kuichapa 2-1.

Nazo timu za kundi D za Ivory Coast, Mali, Cameroon na Guinea zitaonyeshana kazi kazi kesho, Jumamosi. Ivory Coast itaumana na Mali, huku Cameroon ikipambana vikali na Guinea. Timu za kundi hili zina pointi moja moja kabla ya mpambano wao wa mzunguko wa pili.