Tanzania mwenyeji mchezo wa kriketi

Image caption Tanzania kuhodhi michuano ya kriketi kwa wanaume chini ya miaka 19

Tanzania sasa itakuwa mwenyeji wa michuano ya Afrika ya kriketi daraja la 1 kwa wanaume chini ya miaka 19 itakayofanyika February 13 katika viwanja tofauti jijini Dar es Salaam.

Hapo awali, michuano hiyo ilipangwa kufanyika nchini Namibia lakini kwa mujibu wa maofisa wa chama cha kriketi nchini Tanzania (TCA), michuano hiyo imehamishiwa Dar es Salaam.

Kocha wa timu ya taifa, Hamis Abdallah amesema wanaendelea na mazoezi na wanategemewa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kuibuka washindi

Timu kutoka nchi za Namibia, Kenya, Uganda, Nigeria na wenyeji Tanzania zitashindana kwa muda wa wiki moja kupata mshindi.

Tanzania mwaka jana pia ilipewa nafasi ya kuwa wenyeji wa michuano ya Afrika chini ya miaka 19 kwa wanawake ikishirikisha timu kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Botswana na Msumbiji.

Katika miaka ya nyuma, Tanzania pia ilikuwa mwenyeji wa michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ya kufuzu kucheza kombe la dunia kwa nchi za Afrika kwa timu za wanawake na wanaume.

Tanzania imepata nafasi ya kushiriki michuano hiyo ya mwezi ujao baada ya kuwa mabingwa wa michuano ya Afrika daraja la pili kwa wanaume chini ya miaka 19 iliyofanyika mwaka jana huko Lusaka, Zambia.