Real Madrid kujenga kituo cha michezo TZ

Image caption Mjumbe kutoka Real Madrid Rayco Garcia na Mkurugenzi wa NSSF,Ramadhani Dau wakitia saini Hati ya makubaliano

Klabu tajiri duniani, Real Madrid ya Uhispania imesaini hati ya makubaliano na Shirika la hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF) kwa ajili ya kujenga na kuendesha kituo cha michezo kitakachogharimu Shilingi bilioni 16.

Ujenzi huo utajumuisha viwanja vitano vya mpira wa miguu, mabweni ya wachezaji na wageni, maduka na huduma nyingine muhimu .

Pia watajenga uwanja wa gofu wenye mashimo 18 utakaoambatana na ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo la ekari 400 lililopo katika mji uliopangwa kuwa wa kisasa wa Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Makubaliano yalifanyika jijini Dar es Salaam muda mchache baada ya maafisa wa Real Madrid, akiwemo mkuu wa vituo vya kulelea wachezaji wa Real Madrid, Rayco Garcia,ambaye wakati wa uchezaji wake alicheza na Ronaldo de Lima, Roberto Carlos na Zinedine Zidane. Kwa sasa ni kocha wa kikosi cha timu ya Real Madrid chini ya miaka 19.

"Tumefurahishwa sana na mradi huu wa kimaendeleo utakaodumu kwa miaka 18 katika kutafuta, kukuza na kuendeleza vipaji nchini Tanzania kwa ajili ya kutafuta kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya na kwingineko duniani", alisema Garcia.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa NSSF, Ramadhani Dau, hati ya makubaliano ina sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni kazi ya shirika hilo kubwa Tanzania kujenga kituo hicho na sehemu ya pili itakuwa ni ya Real Madrid kuhusika katika kuleta makocha, kusimamia mchakato wa kupata vijana chini ya miaka 13, 14, 15, an 16 watakaoingia katika kituo hicho na kusimamia chakula bora.

Pia itahusika na kutafuta masoko kwa wachezaji hao baada ya kuwatangaza kupitia televisheni ya Real Madrid.

Pia Dau alisema uwekezaji huo utatoa fursa kwa Tanzania kupata wachezaji kwa ajili ya kushiriki kucheza kombe la dunia katika miaka ijayo ili kutimiza ndoto ya muda mrefu.

Tanzania imekuwa moja ya kivutio kikubwa barani Afrika kwa timu za Ulaya. Hiki kitakuwa ni chuo cha pili kujengwa baada ya klabu ya Sunderland ya Uingereza nayo kuendelea na ujenzi wa kituo kingine.

Hivi karibuni, maofisa wa klabu ya Arsenal ya Uingereza pia walitua Tanzania kwa ajili ya kutafuta ubia wa kuuza vifaa vyake vya michezo kama vile Jezi baada ya kugundua kuwa wana wapenzi na mashabiki wengi

Wengine walioambatana na Garcia ni Francisco Martin, Juan Jose Milla (makocha) na mkurugenzi wa ufundi Ruben de La Red.