Tanzania yajipanga kwenda Olimpiki:Gofu

Image caption Mchezaji wa Golfu akiwa uwanjani

Chama cha gofu nchini Tanzania kimetoa kalenda ya mwaka ya 2015 ya michezo ikionesha michuano mbalimbali ikiwemo ya Afrika ya Mashariki Kanda ya 5, ambayo itakuwa ni sehemu ya kufuzu kucheza Olimpiki mwakani mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Gofu na raga itakuwa ni sehemu ya michezo itakayoshindaniwa katika Olimpiki ya mwakani na TGU baada ya kuidhinishwa na kamati ya Olimpiki duniani (IOC) kama sehemu ya michezo itakayoshindaniwa.

Na kutokana na hilo, TGU imedhamiria kupeleka timu Brazil. Michuano hiyo ya kanda ya 5 ya Afrika itafanyika Kigali, Rwanda baadae mwaka huu.

Kabla ya kwenda Kigali, TGU inategemewa kuandaa hafla ya kuchangisha fedha mwishoni mwa mwezi wa tatu mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya timu ya taifa. Uchangishaji fedha pia utafanyika baade kati kati ya mwaka huu

Miongoni mwa michuano ya kimataifa ambayo Tanzania inategemewa kushiriki ni pamoja na michuano ya wazi ya Kenya (Kenya Open) na Coast Open itakayofanyika kati ya February na March, ambayo itakuwa ni kama sehemu ya maandalizi.