Kesi ya upangaji matokeo kutolewa na FIFA

Image caption Boniface Wambura

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limesema matokeo ya uchunguzi wa tuhuma za upangaji matokeo zinazowakabili waamuzi watatu wa Tanzania yatatolewa na shirikisho la dunia, FIFA baada ya uchunguzi kukamilika.

Mkurugenzi wa mashindano wa TFF, Boniface Wambura amesema mara nyingi FIFA inafanya uchunguzi wake kimya kimya bila hata ya chama husika kujua mwenendo ufuatiliaji wake.

“Wakati mwingine unapata tu taarifa wanakuja, lakini wanapomaliza, wanaweza kuondoka bila hata ya kujua na baadae wakaeleza walichokiona baada ya uchunguzi wao”, alisema Wambura.

Kauli ya Wambura inakuja wakati kukiwa na taarifa kuwa maofisa kutoka Fifa wamekuja Tanzania kwa ajili ya kufuatilia sakata la tuhumza za upangaji matokeo zinazowakabili waamuzi

Upangaji wa matokeo katika soka si swala geni, iwe Afrika, Asia au kwingine barani Europa katikia mechi za ligi kuu au mashindano ya kimataifa.

Tanzania ni moja ya nchi iliyokumbwa na tuhuma hizo na tayari ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) upo nchini kuchunguza tuhuma za upangaji matokeo.

Hivi karibuni, TFF ilisimamisha waamuzi kwa tuhuma hizo na kwa mujibu wa Wambura, waamuzi waliosimamishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na watu wengine watahojiwa na ujumbe huo. Matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa na FIFA baada ya shughuli hiyo kukamilika.

Wambura amewaomba wadau wa mpira wa miguu kufuata kanuni na maadili ya TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA katika utendaji wao.

“FIFA itahakikisha kuwa haki inatendeka katika uchunguzi ambao inaufanya”, alisema Wambura.

Waamuzi wanaochezesha ligi kuu waliosimamishwa takriban mwaka mmoja uliopita ni Hamis Chang’walu, Oden Mbaga na Jese Erasmos