Tanzania na michuano kanda ya 5 Afrika

Image caption Beach soka

Tanzania yachagua timu kuzikabili nchi nyingine za Afrika katika wavu,Chama cha mchezo wa wavu (Tava) Tanzania, kupitia kamisheni ya mashindano ya ufukweni, kimetaja timu itakayocheza na timu nyingine kutoka Kenya, Burundi, Sudani Kusini, Rwanda na Somalia katika michuano ya kanda ya tano ya Afrika itakayofanyika kati kati ya mwezi ujao katika fukwe ya bahari ya Mbalamwezi jijini Dar es Salaam.

Michuano hiyo ya kwanza kufanyika Tanzania, itakuwa ni sehemu ya kufuzu kucheza michuano ya Olimpiki itakayofanyika katika mji wa Rio de Janeiro, Brazil mwakani.

Baada ya michuano hiyo, kwa mujibu wa Rais wa Tava, Augustino Agapa, bingwa atashiriki michuano ya Afrika itakayofanyika Lubumbashi baadae mwaka huu katika michuano itakayoshirikisha mabingwa kutoka kanda zote za Afrika ili kupata timu zitakazowakilisha bara la Afrika katika ya Olimpiki ya wavu ya ufukweni dhidi ya mabara mengine.

Waliochaguliwa ni pamoja na Furhani Abubakari, Mohamed Ismail (Kutoka Zanzibar), David Ernest, Ford Edward, Hellen Richard, Evelyn Elbert na Zuhura Hassan.

Wachezaji hawa walichaguliwa katika michuano ya taifa ya wazi iliyofanyika Dar es Salaam mwezi Januari mwaka huu.