Malabo wageuka Uwanja wa Vita

Haki miliki ya picha afp
Image caption Polisi wakijaribu kutuliza ghasia

Nusu fainali za pili za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon kati ya Ghana na wenyeji Equatorial Guinea zinaelezwa kama "ukanda wa vita" baada ya mchezo huo kusitishwa kwa zaidi ya dakika 30 kwa sababu ya ghasia za mashabiki.

Mashabiki kutoka majukwaani waliwarushia chupa za maji wachezaji, na kulazimisha mashabiki wa Ghana kutafuta mahali pa kusitiri maisha yao nyuma ya goli, polisi wa kuzuia ghasia na helikopta iliruka juu ya uwanja kuwatuliza mashabiki lakini hawakufanikiwa.

"Ni kama sasa uwanja wa vita," kiliandika chama cha mpira cha Ghana(GFA) katika ujumbe wake wa tweeter, kikidai kuwepo kwa vitendo vya "kinyama na uharibifu" na "mashambulio ya vurugu kwa jambo lisilo na sababu" yalifanyika ndani ya uwanjani.

Wakati mchezo unarejea, Ghana tayari ilikuwa imefunga magoli 3-0 na kutinga fainali dhidi ya Ivory Coast itakayochezwa Jumapili. Kufika hatua hiyo Ivory Coast, iliifunga DR Congo 3-1 katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa Jumatano.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watazamaji wakijaribu kukimbia

Vurugu zilikithiri katika kipindi cha pili cha mchezo kati ya Ghana na Equatorial Guinea.

Ushindi huo wa Ghana haukuwafurahisha mashabiki wa timu mwenyeji, ambao walikuwa na matumaini makubwa kuona timu yao inacheza fainali ya Jumapili dhidi ya Ivory Coast.

Ghana ilianza kujipatia magoli yake kupitia kwa Jordan Ayew akifunga katika dakika ya 42 kwa njia ya penalti, Wakaso Mubarak dakika ya 45 na Andre Ayew alikipigilia msumari wa moto katika dakika ya 75.

Goli hilo la tatu ndilo lililokuwa limezidisha fujo kiwanjani kwa mashabiki wa Equatorial Guinea kuwarushia chupa za maji wachezaji kiasi cha mpira huo kusimamishwa kwa muda mrefu.

Kwa matokeo hayo Ivory Coast na Ghana ndizo zitakazocheza fainali za Afcon kwa mwaka 2015 siku ya Jumapili zinazofanyika nchini Equatorial Guinea na kutangazwa moja kwa moja na BBC.

Lakini mchezo huo utatanguliwa na ule wa Jumamosi kutafuta mshindi wa tatu kati Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo dhidi ya Equatorial Guinea.