Wenger:Jack Wilshere si mvutaji

Haki miliki ya picha d
Image caption Kiungo wa Arsenal ,Jack Wilshere

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger ameibuka na kumtetea kiungo Jack Wilshere,kuwa mchezaji huyo si ‘’mvutaji wa sigara’’ licha ya picha zake kusambaa katika mitandao ya kijamii akiwa ameshika mrija wa shisha.

Ni mara ya tatu kwa mchezaji huyo kupigwa picha akiwa anavuta sigara katika maeneo mbalimbali ya starehe na picha zake kusambaa katika mitandao ya kijamii.

Wenger amesema mchezaji huyo inabidi aangalie maisha yake ya soka kwani bado ni kijana mdogo mwenye uwezo mkubwa wa kucheza soka,lakini matukio yake ya ajabu yanaweza kumfanya ashindwe kufanya vizuri siku za usoni.

“Hakuna utamaduni wa uvutaji sigara katika kikosi changu, niliongea na Jack kuhusu swala la picha zake zinazoonyesha akivuta na kusema yeye sio mvutaji, lakini inabidi aangalie maisha yake,” alisema Wenger.

Pia wenger amekanusha madai kuwa katika klabu ya Arsenal kuna tatizo kubwa la wachezaji wake kuvuta sigara wakiongozwa na kiungo Wilshere.