Ngasa aomba Yanga imlipie deni

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Ngassa akiwa kazini

Mshambuliaji machachari wa klabu ya Yanga, ameiomba klabu yake kumlipia deni analodaiwa benki ili aweze kucheza kwa bidii na kuwa mfungaji bora.

Ngasa aliamriwa kulipa deni la Sh 45 milioni kwa kosa la kujiunga na Yanga bila kufuata utaratibu akitokea Simba, hivyo , kwa makubaliano, analazimika kukatwa Sh500,000 (wastani wa dola 280) kila mwezi kutoka katika sehemu ya mshahara wake anaoupata kutoka Yanga ili kulipa deni.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, benki , baada ya kukata 500,000, ililazimika kuchukua mshahara wote wa Ngasa katika miezi ya hivi karibuni ili kufidia deni analodaiwa baada ya uongozi uliopita wa klabu hiyo kushindwa kupitisha benki mshahara wake benki kwa muda unaokisiwa mwaka mmoja, hivyo kutolipa kwa mujibu wa makubaliano na benki kulazimika kumuacha mchezaji huyo bila senti.

Ngasa aliripotiwa kusema kuwa hali yake ya kifedha “financial status” ni mbaya na kushindwa kucheza vizuri, na kuiomba Yanga kuangalia namna ya kumsaidia kulipa ili aweze kubakiwa na fedha za kutoka.

“Tutakaa na Ngasa tuangalie namna ya kumsaidia”.

“Licha ya matatizo aliyonayo, ameonesha kuwa ni mchezaji anayejituma na magoli mawili aliyofunga hivi karibuni na kutupa ushindi wa 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika ligi kuu inaonesha anavyoithamin i timu yake”, alisema Muro.

Kutokana na makato yanayomkabili, Ngasa, ambaye mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu wa ligi, alitangaza kuachana na Yanga ili akacheze mpira nje ya nchi, lakini klabu yake imesema itamuongeza mkataba mwingine baada ya mazungumzo ya hivi karibuni.