TFF yapongeza mradi wa Real Madrid

Image caption Raisi wa TFF,Jamal Malinzi

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limetoa pongezi kwa Shirika la Taifa la hifadhi ya jamii (NSSF) kwa juhudi zake za kukuza soka la vijana kupitia mradi wake wa kuanzisha shule ya soka (Academy) kwa ushirikiano na klabu ya Real Madrid ya Hispania.

Afisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto amesema TFF pia inaipongeza kampuni ya Symbion na klabu ya Sunderland ya Uingereza kwa juhudi zao za kuchangia maendeleo ya soka la vijana na mpira wa miguu kwa ujumla ikiwa ni kupitia mpango wa kujenga shule ya soka (academy), uwezeshaji wa mashindano ya vijana chini ya miaka 13 (U-13) yatakayofanyika mwezi April, 2015 mjini Mwanza na ujenzi wa miundo mbinu ya soka na michezo kwa ujumla.

Real Madrid, klabu tajiri barani Uropa kwa sasa, imeingia mkataba wa mabilioni na NSSF na itahusika kuendesha Academy nchini Tanzania yenye lengo la kukuza mpira na kuuza wachezaji barani Afrika na kwingineko duniani.

Mradi huo, ambao umeanza umeelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kupata wachezaji wazuri kwa ajili ya michuano mikubwa mbalimbali kama vile kombe la dunia na michuano ya soka barani Afrika (AFCON).