Kriketi Tanzania yataja kikosi kuivaa Namibia

Image caption Mchezaji akiwa mazoezini

Chama cha Kriketi Tanzania (TCA) kimetaja kikosi cha wachezaji 14 kitakachocheza na Namibia katika moja ya mechi za ufunguzi za michuano ya kufuzu kucheza kombe la Dunia mwakani kwa wavulana waliochini ya miaka 19.

Mechi hizo zitafanyika siku ya Jumapili jijini Dar es Salaam ambapo mbali na mechi kati ya wenyeji Tanzania na Namibia itakayochezwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kenya, watacheza na Nigeria (Uwanja wa Gymkhana) na Uganda watacheza na Botswana (Uwanja wa Annadil Burhani).

Wachezaji wa timu ya Tanzania ni pamoja na nahodha Arshan Jesani, Godluck Andrew, Salum Jumbe, Juma Mohammed, Shafii Kolo, John Ngati na Hamis Said.

Wengine ni Martin Kavuli, Rashid Awadhi, Umang Somanyi, Razaro Festo, Harshened Anant, Suleiman Nassoro, and Raheel Krishna.

Watakuwa chini ya makocha Khalil Rehemtulla na Hamis Abdallah.

Michuano hiyo ni sehemu ya kufuzu kucheza kombe la Dunia litakalofanyika mwakani, Dhaka, Nigeria.