Udanganyifu wa mechi wakumba soka Kenya

Image caption kikosi cha timu ya taifa la kenya Harambee stars

Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Aljazeera umeelezea vile walaghai wa kimataifa huwahonga marefa,wachezaji na maafisa wa mashirikisho ili timu zao ziweze kufuzu kwa michuano kadhaa.

Katika Uchunguzi huo ulionyeshwa na runinga ya Aljazeera tarehe 19 mwezi wa pili mwaka huu,wachezaji watatu wa timu ya taifa ya harambee starts nchini Kenya walipewa hadi dola lali 100,000 kuhakikisha kuwa wanashindwa na Nigeria ili taifa hilo la Afrika magharibi liweze kufuzu kwa michuano ya kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika kusini.

Majina na nyuso za wachezaji hao waliokutana na mlaghai huyo raia wa Singapore katika Hoteli moja jijini Nairobi mnamo mwezi Novemba mwaka 2009 hayakuonyeshwa lakini haitachukua mda kabla majina hayo na maelezo ya kashfa hiyo kufichuliwa kwa wakenya.

Tayari aliyekuwa kocha wa kikosi hicho wakati huohuo Twahir Muhiddin ametaka uchunguzi kufanywa na wachezaji waliohusika kubeba msalaba wao wenyewe.