Kocha:Tumejifunza licha ya kushindwa

Image caption Kocha akitoa mafunzo

Kocha wa kriketi wa Tanzania amesema kikosi chake kimepata uzoefu na kujifunza mengi wakati wa michuano ya vijana chini ya miaka 19 ya kufuzu kucheza kombe la Dunia iliyomalizika Dar es Salaam siku nne zilizopita licha ya kutofanya vizuri.

‘Tulijiandaa ili kushinda, ila wenzetu walijiandaa zaidi na kutuzidi maarifa kidogo”, alisema kocha-mchezaji Khalil Rehemtullah.

“Tulikuwa na matatizo kidogo katika kubeti ila tumejifunza mengi kwa ajili ya michuano ijayo”, alisema Khalil, aliyesomea ukocha Uingereza na kucheza vilabu kadhaa vya huko Ulaya kama vile Watford Town.

Licha ya kufungwa na Kenya kwa runs 125 katika mechi yao ya mwisho , Namibia imefanikiwa kufuzu kucheza kombe la Dunia mwakani huko Bangladesh.

Namibia wamefanikiwa kufuzu baada ya kumaliza michuano ya Daraja la 1 Afrika ya kufuzu ya kucheza kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 19 wakiwa na pointi 8 kutokana na kushinda mechi nne katika michuano ya kufuzu iliyomalizika Dar es Salaam Alhamis.

Uganda walifanikiwa kuwafunga wenyeji Tanzania kwa runs 125 na kumaliza nafasi ya pili, hivyo kupewa nafasi nyingine ya kucheza michuano mingine ya kufuzu ya mabara itakayofanyika Bangladesh baadae mwaka huu.

Michuano hiyo ya mabara itajumuisha timu zote zilizoshinda nafasi ya pili kutoka kila bara ili kutafuta timu itakayofuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani.

Kenya, kufuatia ushindi wao dhidi ya Namibia, wameshika nafasi ya tatu baada ya kumaliza michuano wakiwa na pointi 6 kutokana na michezo mitano waliyocheza, wameshinda mitatu na kupoteza miwili.

Wenyeji Tanzania wamemaliza wakiwa nafasi ya 4 wakiwa na pointi 4 kutoka katika mechi mbili walizoshinda na kupoteza mechi tatu.

Nigeria waliwafunga Botswana kwa runs 9 na kushika nafasi ya 5 wakiwa na pointi 4, baada ya kushind mechi mbili na kufungwa tatu.

Botswana ni timu ya mwisho ikiwa na pointi mbili tu, wakiwa na rekodi ya kushinda mechi moja na kufungwa mechi nne