Yanga na Azam kuelekea Ughaibuni

Image caption Kocha wa timu ya Yanga Plaijm

Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya vilabu barani Afrika, Azam FC na Yanga Africans wanaondoka Jumanne na Jumatano wiki hii kuelekea ughaibuni kwa mechi zao za marudiano.

Azam wataondoka Jumanne kuelekea Khartoum, Sudani kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya wenyeji itakayofanyika Usiku wa Jumamosi.

Msemaji wa Azam, Jafari Idd ameiambia BBC kuwa wanaondoka wakiwa na matumaini ya kushinda na kuwatoa El-Merreikh ili wasonge mbele katika hatua inayofuata.

Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Dar es Salaam, Azam walishinda 2-0 na wanahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili wasonge Mbele.

Hii ni mara ya kwanza kwa mabingwa hawa wa Tanzania kushiriki michuano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Wawakilishi wenza, Yanga nao wanategemewa kuondoka kuelekea Botswana Jumatano kwa ajili ya mechi ya marudiano ya kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup) dhidi ya wenyeji BDF X1 ya nchini humo itakayofanyika pia wikiendi hii.

Yanga nao wanahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili kusonga Mbele. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam, Yanga walishinda 2-0.