wanariadha 5 kuiwakilisha Tanzania China

Image caption Suleiman Nyambui akizungumza na wana riadha.

Chama cha Riadha nchini Tanzania (AT) kimesema kina matumaini kuwa wakimbiaji wa Tanzania watafanya vizuri katika mbio za Nyika za Dunia zitakazofanyika tarehe 28 March mwaka huu nchini China katika mji wa Guiyang.

Wakimbiaji kutoka katika nchi za Afrika, kama vile Kenya,Uganda Ethiopia ,Eritrea, Morocco na nyinginezo wamekuwa wakifanya vizuri zaidi katika michuano hiyo mikubwa na kushinda medali.

Uganda inategemewa kuwa wenyeji wa Michuano hiyo mwaka 2017.

Miogoni mwa miaka ambayo Afrika ilifanya vizuri ni mwaka 2009 katika mbio za Nyika zilizofanyika Amman, Jordan ambapo Gebre Gebremariam wa Ethiopia alishinda katika kilometa 12 akimshinda - Moses Kipsiro wa Uganda na Zersenay Tadese wa Eritrea.

Katika mbio za Kilometa 8 (wanawake), Florence Kiplagat wa Kenya alishinda huku Linet Masai (pia kutoka Kenya) akishinda medali ya fedha na Meselech Melkamu wa Ethiopia akishinda shaba.

Nyambui amesema wanategemea kuchagua wakimbiaji 5 wanaume, baada ya kupewa nafasi na waandaji, ambao watagharamia kila kitu kwa washiriki zikiwemo gharama za usafiri, malazi na chakula.

“Tuna imani wachezaji wetu watafanya vizuri, ikiwa ni sehemu ya kujiweka vizuri kwa ajili ya Michuano ya Afrika (All Africa Games) na Olimpiki itakayofanyika mwakani Rio de Janeiro, nchini Brazil”, amesema Nyambui.