FA:Matamshi ya unyanyasaji yaripotiwe

Image caption Mwanachama wa Bodi ya FA, Heather Rabbats

Chama cha soka England, FA, kimewataka mashabiki kutoa taarifa kuhusu unyanyasaji wa kijinsia katika michezo baada ya kuonekana tukio la kukera dhidi ya maafisa wa kike wa soka kuimbiwa nyimbo chafu. Picha za video zilizopatikana na BBC zinaonyesha kuwa Daktari wa kike wa Chelsea Eva Carneiro na mwamuzi msaidizi Helen Byrne wamekutwa na mikasa ya kudhihakiwa katika mechi za hivi karibuni.

Mmoja wa wanachama wa bodi ya FA, Heather Rabbatts ameelezea unyanyasaji huo kuwa ni tishio na kuongeza kuwa hauwezi kuvumiliwa. '' tunasisitiza watu kutoa taarifa za matukio kama haya'alisema.'

Picha hizo za video zilichukuliwa katika mechi kati ya Chelsea dhidi ya Manchester City na nyingine dhidi ya Manchester United pamoja na mchezo katika mashindano ya Football League yanayoshirikisha vilabu mashuhuri vya England na Wales.

Msimu huu matukio 25 ya udhalilishaji katika mechi zilizochezwa mchana yameripotiwa kwa kikundi kinachopiga kampeni dhidi ya ubaguzi cha Kick It Out na kikundi cha haki kwa Wanawake katika mchezo wa mpira wa miguu (WiF). Msimu uliopita kulikuwa na matukio mawili tu. Hata hivyo kukosekana kwa ushhidi kuna maana hakuna klabu au shabiki ambaye amewahi kuadhibiwa na vyama vya soka.